Chuo cha Ujasiriamali cha Kiafrika cha Ujerumani (AGEA) ni mpango ulioanzishwa na Programu ya kimataifa ya SEPT ya Chuo Kikuu cha Leipzig kwa ushirikiano na washirika wake katika Afrika na Ujerumani. Lengo ni kukuza elimu ya ujasiriamali na kuanzisha viatamizi vya biashara katika Afrika na pia kuanzisha ushirikiano wa vitendo kati ya AGEA na biashara zinazoanza na hata zilizokwishaanzishwa. Kwa kuongezea, AGEA inasaidia biashara zenye mrengo wa Afrika nchini Ujerumani na inatoa msaada muhimu unaohitajika na biashara zinazotaka kufanya biashara katika Afrika.
AGEA imeanzishwa ili kuziwezesha taasisi za elimu ya juu katika shughuli za kukuza ujasiriamali na kuanzisha viatamizi vya biashara katika Afrika. Pia ni jukwaa la kuhamasisha kushirikishana ujuzi miongoni mwa taasisi za elimu ya juu za Kiafrika pamoja na sekta binafsi. Aina hii ya ushirikishanaji ujuzi inafanywa kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya Ujerumani na vyama vya kibiashara (uhamishaji wa ujuzi kati ya Kusini na Kusini na ushirikiano kati ya Kaskazini na Kusini).